1 Juni 2024 - 19:52
Biden atangaza mpango wa kukomesha vita Ghaza, Netanyahu asisitiza vita vitaendelea

Ofisi ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu imesisitiza juu ya nia ya serikali ya Netanyahu ya kuendeleza mashambulizi ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Ghaza hadi itakapohakikisha malengo yote ya vita ya Tel Aviv yamefikiwa.

Sisitizo hilo limetolewa mara baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kutangaza pendekezo jipya la kusitisha vita ambalo amesema limeidhinishwa na Israel na kuitaka harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ilikubali. Ofisi ya Netanyahu imeendelea kusema: "vita havitakwisha hadi malengo yake yote yafikiwe, ikiwa ni pamoja na kurejea kwa mateka wetu wote na kuangamizwa uwezo wa kijeshi na kiutawala wa Hamas." Hata hivyo taarifa ya ofisi hiyo imeongeza kuwa, Netanyahu ameipa idhini timu ya mazungumzo ya Israel "kuwasilisha muongozo wa kufikia lengo hilo," akimaanisha kukombolewa mateka.Pendekezo hilo lililotangazwa na Biden, litatekelezwa kwa awamu tatu, ya kwanza ikichukua wiki sita na kujumuisha usitishaji vita kamili, kuondolewa vikosi vya jeshi la Kizayuni kutoka maeneo yenye watu wengi huko Ghaza, na kubadilishana mateka.

 Mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Israel na Hamas, yaliyofanyika kwa upatanishi wa Marekani, Qatar na Misri, hadi sasa yameshindwa kufikia mwafaka juu ya usitishaji vita wa kudumu. Tangu Oktoba 7, 2023 hadi sasa jeshi la utawala haramu wa Kizayuni limewaua shahidi zaidi ya Wapalestina 36,240 huko Ghaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine zaidi ya 81,777 wamejeruhiwa.../

342/